KONYAGI

Friday, October 7, 2016

KIZUNGUMKUTI CHA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA HAKIMILIKI


Hakika neno Hakimiliki si jipya kwa wapenzi wa muziki nchini. Lilianza kuwa maarufu miaka ya tisini wakati biashara ya kanda za kaseti imeshamiri. Wanamuziki walianza harakati za kudai Hakimiliki kwa sauti zaidi baada ya kuanza kuona kanda zao zinauzwa lakini hawapati chochote. Je, Hakimiliki ni nini?
Hakimiliki ni haki anazopewa mtunzi ili kuweza kulinda maslahi yake katika tungo zake. Tungo ni mali, lakini mali hii bahati mbaya ikishatoka hadharani ni vigumu kuzuia wengine kutumia. Hivyo ili kulinda maslahi ya mtunzi kumetengenezwa sheria za Hakimiliki, sheria zinazompa mtunzi haki kuu mbili, haki za kimaadili na haki za kiuchumi. Haki za kimaadili, ni zile haki zinazolazimisha mtunzi kutajwa wakati kazi yake inapotumika. Hivyo basi jina la mwandishi wa kitabu linapoonekana juu ya kitabu, ni katika kutimiza haki za msingi za mtunzi kwa kujulisha kuwa tungo ile ni mali yake, au majina ya wasanii wa filamu kuonyeshwa mwanzo au mwisho wa filamu ni katika kutekeleza haki hii, na hata mwanamuziki kutajwa juu ya jarada la kazi yake ni katika kutimiza haki hii. Haki ya pili ni kundi la haki za kiuchumi. Haki hizi kumuwezesha mtunzi kupata pato la kiuchumi kutokana na kazi yake. Hivyo anakuwa na haki ya kurudufu kazi yake,kusambaza, kutafsiri, kuazimisha, kuitangaza katika vyombo vya utangazaji, kuibadili matumizi na kadhalika na katika njia hizi mbalimbali za matumizi akapata malipo kutokana na kazi yake. Kwa kuwa mtunzi anaweza kuwa hana uwezo wa kurudufu na kusambaza, huingia makubaliano na wasambazaji kwa kuwapa haki yake ya usambazaji, ili wasambaze kazi yake nae apate mgao wake. Hivyo kusambaza kazi bila makubaliano na mwenye kazi ni kumnyima haki mwenye kazi. Kwa kuwa mtunzi wa muziki anahitaji kazi yake isikike, hutoa haki ya kazi yake kutangazwa kwenye vyombo vya habari, lakini kwa kuwa vyombo vya habari hutumia kazi ile kupatia wasikilizaji zaidi kwenye vyombo vyao na hivyo kuvutia watangazaji, na hata kutumia katika vipindi vinavyoingiza fedha, mtunzi hulazimika kulipwa mirabaha, ambayo ni asilimia ndogo ya pato la vyombo vya habari kama stahili yake katika biashara hiyo. Vivyo hivyo iwapo kazi ya utunzi itatumika kwenye biashara ya muziki katika simu kama ‘ringtones’ au ’caller tunes’ na kwa kuwa kuna fedha hupatikana, mwanamuziki anastahili kupata mgao wake wa biashara hiyo, na utaratibu huo hutumika popote pengine ambapo tungo hutumika na yakafanyika malipo. Kwa muda mrefu swala hili limekuwa likigusiwa na viongozi mbalimbali wakitoa mifano ya wanamuziki wa nchi nyingine kufaidika na kazi zao lakini bado kimekuwa kitendawili kwa wanamuziki wa hapa nchini, ambao wengine hufa kwa dhiki japo kazi zao zinaingiza fedha kwa njia moja au nyingine. Tatizo liko wapi? Tatizo kubwa la kwanza ni kuwa hakuna nia thabiti ya kubadili hali ilivyo. Hivyo hatua kali za kudhibiti dhuluma kubwa wanayofanyiwa wanamuziki na wasanii wengine kupitia kudhulumiwa haki zao hazichukuliwi. Mwaka 2001 ilitengenezwa kamati iliyoitwa National Anti Piracy Committee, kamati ambayo kazi yake ilikuwa ni kutengeneza kanuni zitakazoweza kudhibiti wizi wa kazi sanaa za video na audio. Kamati hii ilitengeneza kanuni ambazo ziliongoza kuwa kila CD, DVD na vifaa kama hivyo ambavyo vinakazi za sanaa na vinatakiwa kuuzwa, lazima view na stika ya COSOTA. Stika hii ilipewa jina la Hakigram, na mwaka 2005 kanuni hii ilisainiwa na Waziri wa Viwanda na Biashara wakati ule na kuwa tayari kutangazwa katika gazeti la serikali ili kuwa sheria halali. Karatasi zenye saini ya Waziri zilipotea katika mazingira ya kutatanisha kabla ya kutangazwa!! Mwaka uliofuata COSOTA iliwezesha mchakato kurudiwa kupitia Waziri  wa kipindi hicho na hatimae sheria ikapitia taratibu zote na kuwa rasmi. Baada ya hapo COSOTA ilianza jitihada kuiomba serikali kutoa fedha za kuanza kufanikisha taratibu hizi za kisheria kwa kununua stika za awali, pamoja na maneno mazuri sana ya viongozi mbalimbali kuonyesha kuwaonea huruma wasanii kwa kuibiwa , lakini fedha hazikutolewa kwa shughuli hiyo mpaka leo hii. Mwaka 2007 zikaanza harakati nyingine za kutengeneza sheria ya kuweka stika kwenye CD na DVD ila awamu hii stika hizo zilikuwa ni za TRA. Zaidi  ya mara moja ilitangazwa na viongozi wa juu kuwa serikali ilitoa shilingi milioni 20 kwa ‘mtaalamu’ toka Chuo Kikuu Dar es Salaam ili kufanya utafiti ambao uliwezesha serikali kuanzisha utaratibu wa stika ya TRA ambao utaratibu huu ungemaliza wizi wa kazi za muziki na filamu. Mpaka leo ‘Mtaalamu’ hajulikani jina wala ‘utafiti’ haujulikani uko maktaba gani. Lakini sheria iliyoitwa ‘The Films and Music Products (Tax Stamps) Regulation, 2013’ iliweza kupatikana. Ni mwaka wa tatu sasa sheria hii ipo, wizi uko palepale, mbaya zaidi kutokana na utekelezaji wa sheria hii, uuzaji halali wa CD na DVD za  wanamuziki wa Tanzania ndio umetoweka kabisa,  wasambazaji wamekimbia kwa maelezo kuwa biashara hiyo hailipi tena. Matokeo ya kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo iliyofanyiwa ‘utafiti wa milioni 20’.
Mwaka 2003, ilipitishwa kanuni ambayo ilielekeza utekelezaji wa vyombo vya utangazaji, radio na TV kulipia kazi za muziki zinazorushwa na vyombo hivyo.  Kanuni hii inayoitwa ‘The Copyright (Licensing of Public Performances and Broadcasting) Regulations 2003’ ilitangazwa kwa mara ya kwanza , tarehe 10 Oktober 2003, ina miaka 13 sasa, na bado hakuna kinacholipwa. Hakika umefika muda muda sasa hadithi ziishe kazi ianze, hebu fikiria nchi nzima zimejaa DVD za filamu zisizo halali na CD za muziki zisizo halali na zinauzwa hadharani, biashara ya kuingiza muziki kwenye flash na memory card bila ruksa ya wenye muziki haifanywi kifichoni nini kinakwamisha sheria isifuatwe?Saturday, August 16, 2014

ULAZIMA WA MILIKI BUNIFU KUTAJWA KATIKA KATIBA


Katika Rasimu ya Katiba kumetajwa ulinzi wa mali, lakini ni wazi mali hizi ni zile zililzozoeleka katika akili za watu mali zinazohamishika na zisizohamishika. Kuna aina ya tatu ya mali ni ile inayotokana na ubunifu, na kwa sasa ndio mali inayolindwa zaidi na mataifa mengi, kwani ndio inayoleta ugunduzi wa madawa, mitambo, teknolojia, sanaa, na maendeleo ya kila aina. Hii huitwa Milikibunifu. Ni muhimu kutajwa kama zilivyofanya nchi nyingine ambazo zimefaidika sana na kulinda milikibunifu za wananchi wake.....
Milikibunifu au Intellectual Property Rights ni haki anazopewa mbunifu ili kulinda hali za mali yake ambayo haishikiki. Mali hii iyokanayo na ubunifu ni muhimu kuilinda kwani matokeo ya mali hii huwa faida kubwa kwa jamii. Milikibunifu ndizo haki ambazo huwalinda wagunduzi wa maendeleo katika teknolojia, madawa ya binadamu mifugo na kilimo, njia mbalimbali za kuongeza ubora na ufanisi wa teknolojia. Milikibunifu imegawanywa katika makundi mbalimbali ya ulinzi;
i.                Patent – (Hataza) hii ni njia ya kulinda na kusajili uvumbuzi mbalimbali wa kiteknolojia. Mfano vifaa vya kuvunia mazao kwa haraka zaidi, au kulima kwa haraka zaidi, vifaa vya uvuvi wa haraka, vifaa vya mawasiliano na vifaa vyovyote ambavyo vitaongeza thamani ya maisha yetu. Katika nchi kama Korea ya Kusini ulinzi wa Milikibunifu uliwekwa katika Katiba kuanzia baada ya vita ya pili ya dunia kwa kufusts mfumo wa  Katiba ya Marekani na ulinzi huo umeifanya wananchi wake ambao ni wabunifu kuweza kuja naubunifu ambao unatikisa dunia vifaa kama Samsung, Daewoo, KIA, LG ni matokeo ya ulinzi wa kikatiba wa wa Milikibunifu
ii.              Trademarks – (Alama za Biashara ) Alama za biashara huweza kufikia hatua ambapo zikawa na thamani kubwa kwani huweza kuaminika. Ili kulinda zisitumiwe hovyo au hata kuibiwa na wenye uwezo zaidi hulindwa na sheria za kulinda alama hizi. Kwa mfano Cocacola, Vodacom, Dell, na hapa kwetu Azam, ni majina ya bidhaa ambazo zina aminika, na hivyo kuwa na dhamani kubwa japo hazishikiki, nazo ni sehemu ya mali  ambazo hazishikiki lakini zina thamani kubwa
iii.             Industrial designs – Hizi ni haki wanazopewa wale wenye ubunifu wa kuweza kufanya usanii wenye kuboresha muonekano wa kitu ambacho tayari kimeshagunduliwa. Kwa mfano kila mtu ana simu ya mkononi lakini muonekano wa simu mbalimbali shape nap engine hali ya kuwa ni ya ku slide au kufungua au kupokea moja kwa moja ni matokeo ya design, pia vitu kama design za nguo, viatu , kiti ulichokalia makochi magari, vyote hivyo ndivyo matokeo ya industrial designs. Kazi za ubunifu huo ni muhimu kulindwa kwani huwa na thamani kubwa sana, kwa mbunifu na kwa mchango wake kwa nchi.  
iv.             Geographical Indication – Huu ni utambulisho wa wapi chanzo cha mali husika. Kwa mfano mvinyo kutoka Dodoma, Dodoma Wine ni mzuri na hivyo huitwa Dodoma Wine bila kulinda hili, watu watachukua mvinyo huu na kuupa hata jina jingine ukaitwa South African wine na hivyo kuiba haki wanazostaili kupata wakulima wa Dodoma, kutambuliwa kwa jina hili kutasababisha kutakiwa zaidi kwa wine hii duniani na hivyo kuweza kufanya hata Dodoma kuwa Wine City jambo ambalo linawezekana lakini nchi haijatambua umuhimu huu. Pia kuna mchele wa Kyela, Dagaa wa Kigoma na vitu kama hivi ambavyo havipatikani popote duniani kasoro sehemu iliyotajwa.  Nchi kama Uswiss imejenga jina miaka mingi ya utengenezaji wa saa bora hivyo saa ikiandikwa Swiss made huwa inajulikana ni bora na huwa gharama zaidi, Sigara kutoka Cuba, Cuban Cigars ni bei kubwa kwani hazipatikani popote kasoro Cuba, au mvinyo maarufu kama Champagne, ambao hutoka jimbo la Champagne Ufaransa, umejijengea sifa kubwa duniani na kuwa na bei kubwa sana kiasi cha kwamba si rahisi kwa mtu wa kipato cha kawaida kununua. Harusi zetu hutumia Sparkling Wine na kuiita Shampeni.
v.              Hakimiliki na Hakishiriki – Hizi ni haki zinazolinda kazi za kisayansi na kisanii. Computer Programs, Data, Utunzi wa vitabu, miswaada, hotuba, uchoraji, muziki, kazi za usonara, picha za mnato na filamu, uchongaji na kadhalika. Kazi hizi zimekuwa ni chanzo cha utajiri mkubwa kwa watu binafsi na Mataifa. Katika nchi ya Marekani kazi za Hakimiliki na Hakishiriki ni za pili katika uchangiaji wa pato la Taifa. Ripoti ya WIPO ya 2010 ilionyesha kuwa katika nchi ya Tanzania kazi za hakimiliki na Hakishiriki zilichangia asilimia 4.3 ya pato la taifa, karibu mara mbili ya mchango wa Madini!. Katika mwaka 2009 kazi za hakimiliki zilitengenza aslimia 5.63 ya ajira nchini, ikiwa juu ya mchango wa Afya (4.23), Biashara na mambo ya Fedha Real estate, &Business Service(2.37), Ujenzi (1.38),Usafirishaji na Mawasiliano (0.92), Umeme, Gas na maji (0.91), Madini (0.89)
Pamoja na umuhimu huu, Katiba inataja mali zinazoshikika tu-Zinazohamishika na zisizohamishika, hivyo mali hizi ambazo zimeonyesha kuleta maendeleo makubwa kwa nchi ambazo wakati wa Uhuru tulikuwa sawa kwa mfano Thailand, India, Malasia, Korea kusini ambazo zote zimetuacha mbali ni kwa ajili ya ulinzi wa mali hizi zisizoshikika ambazo ndizo pia zinawezesha mazingira ya kuingiza fedha nyingi za uwekezaji kutoka kwa wenye pesa na kuanzisha viwanda vyenye mali ya asili ya hapa. Nchi zote zinazoendelea ambazo ziliwahi kuona umuhimu wa kuweka kipengele cha miliki bunifu katika Katiba yake mapema, zimeweza kupata maendeleo ya haraka kama nilivyotaja hapo juu.

 Mifano ya nchi nyingine….
Marikani ni nchi moja wapo ambapo ulinzi wa Milikibunifu umewezesha maendeleo makubwa katika sanaa na teknolojia,
·      U.S. Constitution. Article I, Section 8 provides: "The Congress shall have Power … To promote the Progress of Science and useful Arts, by securing for limited Times to Authors and Inventors the exclusive Right to their respective Writings and Discoveries."
·      The Constitution of Malaysia, which is the supreme law of Malaysia, was adopted on 31 August 1957. Since then, the Constitution has been amended many times, most recently in 2009.
The Constitution contains provisions on intellectual property.
In the Legislative Lists (List I-Federal List) of the Ninth Schedule, the Constitution gives the federal government the power to enact laws relating to patents, designs, inventions, trade marks and mercantile marks, copyrights (Section 8 (e)).
·      Article 22 ya Katiba ya South Korea inasema (1) All citizens shall enjoy freedom of learning and the arts. (2) The rights of authors, inventors, scientists, engineers, and artists shall be protected by Act

Friday, May 30, 2014

DIRECTOR GEORGE TYSON HATUNAE TENA

TASNIA YA FILAMU IMEPATA PIGO JINGINE BAADA YA MUONGOZAJI MAARUFU GEORGE TYSON KUPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI ILIYOTOKEA AKIWA NJIANI KUTOKEA DODOMA KIASI CHA SAA MOJA USIKU 30 MAY 2014. GEORGE ALIWAHI KUWA MUME WA MWIGIZAJI MAARUFU MONALISA NA WAKAPATA MTOTO WA KIKE SONIA. MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI AMEN

Friday, February 28, 2014

Thursday, February 27, 2014

UDHALILISHWAJI WA MSANII HUYU HAUWEZI KUPITA BILA KUKEMEWA

HAIKUSTAHILI YALIYOTOKEA KUISHIA KUSAMBAZWA MTANDAONI. MHESHIMIWA USTAZ JUMA UMETUDHALILISHA WASANII WOTE KWA HILI. PAMOJA NA YOTE ALIYOKUFANYIA, ADHABU HIIYA KUDHALILISHA BINADAMU MWENZIO MTANDAONI NA AMBAYO ITADUMU MPAKA PALE VIDEO HII ITAKAPOONDOLEWA MTANDAONI, ITAKUJA KUKURUDIA SIKU MOJA.

Sunday, February 23, 2014

MAPENDEKEZO YA WASANII KATIKA RASIMU YA KATIBA MPYA.

 Utangulizi
Baada ya maagizo kutoka Tume ya Katiba ya kuwa kila kundi kutayarisha mapendekezo ya rasimu ya Katiba, wasanii nao chini ya mashirikisho yao manne Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Muziki, Shirikisho la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za ufundi  waliweza kuja na mapendekezo kadhaa ambayo waliyawasilisha katika Tume, kwa bahati mbaya hakuna kipengele chochote cha mapendekezo hayo kilicho ingizwa katika Rasimu ya Katiba. Kwa ushirikiano, Mashirikisho haya ya sanaa yameamua kufikisha mapendekezo yao moja kwa moja kwa Wabunge wa Bunge la Katiba ili kuwezesha vipengele hivyo kuweko katika Katiba yetu mpya.
 Mapendekezo
1.    Kutambuliwa kwa wasanii kama kundi maalumu katika Katiba.
Katika Rasimu ya Katika kuna makundi maalumu kadhaa ambayo yametajwa, kama vile wakulima, wavuvi, wafugaji, na kadhalika  na hivyo kutambuliwa kikatiba. Wasanii ni kundi kubwa katika jamii ya Kitanzania. Wasanii wapo karibu katika kila kaya Tanzania. Wafinyanzi, wasusi, wapambaji, wanamuziki waigizaji, mafundi mbalimbali wa ushonaji ujenzi na kadhalika, wako wengi wala hata wao hawajitambui kama ni wasnii kutokana na mazingira waliyomo. Katika ripoti mojawapo ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati huo ilikuwa ni milioni 6, ni wazi kuwa idadi hiyo kwa sasa itakuwa imepanda.  Katika miaka ya karibuni vijana wengi wamekuwa wanaongezeka kujiunga na kundi hili kwani katika sanaa kumekuwa na uwezekano wa kujipatia ajira, tena isiyokuwa na ukomo. Na hivyo sanaa kwa sasa si utamaduni peke yake bali ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania. Wasanii ni sehemu muhimu katika sekta ya Hakimiliki, takwimu za ripoti ya WIPO(World Intellectual Property Organisation) ya mwaka 2010, kuhusu mchango wa sekta ya hakimiliki katika uchumi wa Tanzania, inaonaonyesha  kuwa sekta hii, kati ya 2007-2010 ilichangia kati ya asilimia 3-4.6% ya gross domestic product(GDP). Na kiasi cha kati ya TSH 38.930 bilioni na 86.686 billion kilipatikana kama kipato cha walioajiriwa katika sekta hiyo. Kati ya watu 28, 202 na 44, 331 waliajiriwa rasmi, na hiyo ilikuwa kati ya asilimia 4.5 na 5.2% ya kundi zima la waajiriwa wa Taifa hili. Kwa kipimo cha GDP, sekta hii ilikuwa zaidi ya sekta ya madini, ambayo wote ni mashahidi imekuwa katika mazungumzo kila kona ya nchi. Na katika ajira sekta hii ilikuwa juu zaidi ya sekta nyingi zikiwemo madini, usafirishaji, mawasiliano, afya na ustawi wa jamii, maji, gesi, na hata ujenzi. Kwa mchango wa sekta hii wa 3.2% katika GDP kwa mwaka 2009 , umeweka sekta hii kuwa bora kuliko sekta za aina yake katika nchi  kama Croatia 3%, Singapore 2.9%, Latvia 2.9%, Lebanon 2.5%, Kenya 2.3%. Na katika mchango wa ajira sekta hii ilikuwa juu ya Romania, Bulgaria, Lebanon, Jamaica, Colombia, Kenya na Ukraine. Takwimu hizi hazijionyeshi katika takwimu za serikali kwa kuwa sanaa bado inaonekana ni utamaduni tu, na thamani yake katika uchumi haitiliwi uzito. Kutambuliwa kwa kundi hili kutawezesha kutungwa sheria na taratibu za kuwezesha Wasanii kuongeza ajira na mapato, na Taifa kufaidika na uchumi wa  raslimali hii.
2.     Kutajwa kwa  MilikiBunifu Intellectual Property ) katika Katiba.
Mali ziko za aina 3. Kuna mali zinazohamishika, mali zisizohamishika na mali zitokanazo na ubunifu. Aina mbili za kwanza zimetajwa katika katiba na ulinzi wake hujulikana na ni wa jadi. Lakini hii aina ya tatu ya mali huwa ni ngumu kuilinda kutokana na mfumo wake kuwa haushikiki hivyo sheria maalumu hutungwa kulinda aina hii ya mali (IP Laws). Mali zitokanazo na ubunifu kwa sasa ndio mali zenye kipa umbele duniani. Uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali, ugunduzi wa njia mbalimbali za kuboresha maisha, sanaa na mengi yanayolindwa na milikibunifu, vimeweza kutoa ajira kubwa na kutoa mchango mkubwa wa kipato kwa wagunduzi na nchi ambazo wagunduzi hao wamekuwa wakiishi au kuzisajili kazi zao. Kama wasanii, haki zetu katika milikibunifu zinajulikana kama Hakimiliki, lakini kama Watanzania tunaona ni muhimu kulinda haki zote za Milikibunifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nchi zote ambazo zimeweka taratibu imara za kulinda Milikibunifu duniani, zimewezesha wabunifu wake kubuni mambo ambayo yameweza kubadilisha maisha ya binadamu wengine duniani kote. Marikani iliweka kipengele cha Ulinzi wa hakimiliki katika katiba yake tangu mwaka  Agosti 1787, na kazi za wagunduzi wa Marekani tunaziona kila wakati katika kazi za sanaa na teknolojia. Korea kusini ilinakiri sehemu ya katiba ya Marekani kuhusu ulinzi wa Milikibunifu kuanzia mwaka 1948, kwa wakati huu wote ni mashahidi wa bidhaa kama Samsung, Ld Daewoo, Hyundai na kadhalika.
Milikibunifu pamoja na kulinda haki katika kazi za sanaa ambazo picha ndogo ya mapato yake zimetajwa hapo juu, Milikibunifu italinda haki za wabunifu wetu, tafiti za wasomi wetu, ugunduzi mbalimbali, taratibu mbalimbali za mambo yetu ya kiasili, dawa za asili za miti yetu, na taratibu za matumizi ya dawa hizo, na mali asili zetu nyingine nyingi tunazozifahamu na ambazo bado hatujazifahamu .
Kuna hasara nyingi ambazo hupatikana kama nchi haina ulinzi wa Milikibunifu, mifano michache hapa Tanzania, ni kupoteza kwa Milikibunifu ya jina Tanzanite, ambayo licha ya kuwa inachimbwa Tanzania tu lakini jina linamilikiwa na kampuni ya Afrika ya Kusini. Vazi la kikoi, pamoja kuwa ni la asili ya Tanzania, milikibunifu imesajiliwa Kenya, staili ya michoro maarufu ya Tingatinga milikibunifu yake iko Japan. Na haya ni machache ambayo yameshitukiwa Milikibunifu ikifuatiwa vizuri ndipo haswa ukubwa wa tatizo utakapojulikana. Kuna ulazima mkubwa wa kutaja Milikibunifu katika katiba na kuanisha ulazima wa kulinda kuendeleza na kwezesha wabunifu wan chi kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo