Saturday, March 17, 2012

Katika bendi, wimbo mali ya nani?


Kwa wafuatiliaji wa mambo ya muziki watakumbuka kuwa si mara moja ambapo kumekuweko na uvutano wa nani mwenye wimbo hasa pale ambapo mtunzi kwa sababu moja au nyingine kahama bendi. Nakumbuka niliwahi kuona kisanga hiki mara mbili wakati niko Vijana Jazz Band ambapo mara ya kwanza mwanamuziki mmoja ambaye alikuwa kaacha bendi siku nyingi alipoingia kwenye ukumbi akakuta bendi ikipiga wimbo ambao alitunga, akanza kupiga kelele kuwa bendi iache kupiga wimbo wake, kwani alikwishaacha bendi, tena aliacha kwa kufukuzwa. Japo kuwa Vijana Jazz ilikwisha kuurekodi wimbo huo kitambo. Mara ya pili pia ilitokana na mwana muziki mmoja ambaye yeye aliacha bendi kwa kupenda, kwani alisafiri kwenda nje ya nchi, na siku hiyo akaingia ukumbini na kukuta Vijana Jazz na Super matimila wakipiga pamoja. Vijana Jazz walikuwa wakipiga wimbo ambao yeye ndiye alitambulika kama mtunzi. Alichukua wireless mic kutoka kwa Dr Remmy na kuanza kutangaza kuwa wimbo unaoimbwa ni mali yake na kuanza kuimba katikati ya wimbo jambo lililozua ugomvi mkubwa na wanamuziki wengine wa Vijana Jazz wa kuanza kutukanana kwenye vipaza sauti. Sikinde nao walikuwa na ugomvi wakati Ramadhani Kinguti System alipoacha Bicco Stars na kuhamia Mlimani park Orchestra,  na ‘kuhama’ na wimbo wake.

Je, wimbo mali ya nani hasa? Katika bendi zetu nyingi, wimbo hutajwa kama mali ya mtunzi hasa wa maneno au mashahiri ya wimbo husika. Hivyo basi kuna watunzi huja na mashahiri peke yake au wengine mashahiri yenye sauti ‘melody’, na hata watunzi wengine hasa wapiga vyombo huja na wimbo wenye japo njia za chombo anachopiga kama ni kinanda au gitaa. Wimbo ukisha fika kwenye bendi, hapo huanza kuchangiwa na wanamuziki wote. Waimbaji watapanga sauti, na hata kubadili baadhi ya maneno, mpiga solo atatunga solo, mpiga bezi atatunga bezi mpiga kinanda atatunga kinanda alimuradi kiukweli wimbo huwa ni kazi ya watu kadhaa katika bendi. Kuna bendi ambazo ni mali ya mtu au kundi la watu ambao hugharamia vyombo vinavyotumika katika mazoezi, na kuwalipa hata mishahara wote walioko katika bendi, na hata wakati wimbo unatungwa , toka mtunzi mpaka wanamuziki wengine wote huwa katika ajira na hudai malipo kwa kufika katika mazoezi hayo. Akili ya kawaida tu inaonyesha kuwa wimbo uliokamilika si mali ya aliyeleta mashahiri peke yake, mwenye bendi anahusika, na wanamuziki wengine wengi wanahusika na kuufanya wimbo uwe ulivyo baada ya kukamilika. Sheria ya Hakimiliki ya Tanzania inasema ikiwa umeajiriwa na katika ajira yako ukatunga kazi, kama hakuna makubaliano tofauti na mwenye mali hiyo anakuwa muajiri. Ni vizuri wanamuziki waelewe hilo.

Kwa mfano katika wimbo ambao mwanamuziki aliukatisha kwa kutumia Microphone ya Dr Remmy, mwenyewe aliuleta ukiwa na beti mbili akiuuita Mama Sungura, jina ambalo lilikataliwa na wanamuziki wenzie mara moja, na wimbo ukatengenezwa vizuri na hatimae kuitwa Mama Chichi.

Mara nyingi wanamuziki huenda bendi mpya na kuendelea kupiga wimbo walioutunga zamani, hii huwezekana na katika malipo bendi yake ya zamani hulipwa kwa njia ya vyama vya hakimiliki kukusanya mirabaha kutoka kwenye sehemu ambazo hupiga muziki. Ila kurekodi ni lazima kuweko na makubaliano na bendi ya zamani hasa kama kinachokuja fanyika ni remix ya wimbo wa zamani.

No comments:

Post a Comment